Murphy hakupenda kupoteza muda. Alinyanyuka na kumimina risasi, Mungu akamsaidia akadondosha wawili huku wengine wakipotea kwa kuruka vibaya na kukwepa. Kwa kasi Murphy alikimbia huku ameinama mpaka katika milango mikubwa ya nje, ambayo sasa ilikuwa wazi. Hapo akasita. Chochote kingeweza kumpata kwa nje kama hangekuwa mwangalifu. Bunduki yake ilishakwisha risasi. Aliitupa na kuchungulia nje akaona adui mmoja akikatisha kwenda nyuma ambako ndiko mashambulizi yalikokuwa yakisikika sasa. Murphy hakumtaka huyo. Aligeukia ndani kuona kama kulikuwa na bunduki aichukue lakini hata kisu hakikuwepo. Akiwa bado anashangaa, ghafla alitokea adui – kwa ndani – na kurusha risasi, bahati nzuri akamkosa Murphy. Murphy, kama mbayuwayu, aliruka na kusafiri hewani hapohapo akadondoka nyuma ya tangi la gesi karibu na milango ya nje. Alipoona vile, adui alidhani Murphy alidondoka mbali. Alibung’aa asijue la kufanya. Wasiwasi ulipomzidi alishindwa kuvumilia. Alishika bunduki kwa nguvu na kupiga kelele, "Yuko hukuuu!" Halafu akajificha ili Murphy asimwone. Lakini Murphy alikuwa akimwona.

Related Quotes