Taabini hii ni ngumu sana kwangu kuandika pamoja na kwamba ni miaka mitatu kamili toka giza liingie. Mwaka 2014, Novemba 4, nilimpoteza bibi yangu mpendwa, Martha Maregesi, aliyefariki dunia kutokana na ukongo wa kiharusi, na tutamkumbuka daima.
Alikuwa na roho ya kipekee; na kifo chake kiliwagusa wengi, pamoja na kwamba aliishi maisha kamili, zaidi ya siku 25550, siku 5110 zaidi, ambazo ndizo tulizopangiwa na Mungu.
Mapenzi ya mtu kwa bibi yake ni mapenzi ya kipekee. Nadhani Mungu aliwapa mabibi wote uwezo maalumu wa kuwapenda wajukuu zao, na kufanya maisha yao yatimie, kuwafanya wawe binadamu wazuri na wenye maadili mema.
Alichangia pakubwa katika malezi yangu ya utotoni; na aghalabu naweza kukumbuka nikiwa naye jikoni akipika, huku mimi nikifanya kazi nyingine, lakini wakati huohuo akinifundisha mambo kadha wa kadha ya kunikomaza kimaisha. Bibi hakuwa tu bibi. Alikuwa mlezi, rafiki na mtu aliyenihamasisha sana katika maisha.
Kifo kinaleta huzuni lakini kinaleta tumaini. Naamini bibi yangu atakwenda mbinguni, kwa sababu naamini alitubu dhambi zake akisaidiwa na wachungaji. Wachungaji hao walimtembelea kila siku, nyumbani au hospitalini, akiwa kitandani kwake akiugua. Bibi yangu alitimiza wajibu wake. Alizaliwa, aliishi, na alikufa katika toba.
Siku nitakapokufa ningependa kuzikwa jirani na alipozikwa bibi yangu, ili Yesu atakaporudi tufufuke pamoja.