Bibi Martha Maregesi aliishi maisha mazuri sana hapa duniani. Alibarikiwa na Mungu. Aliishi miaka 84 – siku 30660 badala ya siku 25550 tulizopangiwa na Mungu. Katika uhai wake wote, kwa wale wote aliowalea, hakuna mtoto wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna mjukuu wake hata mmoja aliyefariki kabla yake. Hakuna kitukuu chake hata kimoja kilichofariki kabla yake. Bibi yangu ametimiza mwaka mmoja kamili leo hii, tangu amefariki dunia Novemba 4 mwaka 2014 mjini Musoma. Tunamkumbuka leo akiwa amefariki kama tulivyomkumbuka jana akiwa hai. Nguvu ya sala zetu imfanye Mwenyezi Mungu aendelee kumsamehe dhambi zake zote, na amweke mahali anapostahili, Amina.

Related Quotes

Jina langu ni Enock Maregesi na ningependa kukwambia kisa kidogo kuhusiana na bibi yangu, Martha Maregesi. Mwanamke huyu alikuwa mke mwenye upendo usiokuwa na masharti yoyote. Alikuwa mama na bibi aliyefundisha familia yake umuhimu wa kujitolea na umuhimu wa uvumilivu. Ijapokuwa hakupendelea sana kujizungumzia mwenyewe, ningependa kukusimulia kisa kidogo kuhusiana na hadithi ya maisha ya mwanamke huyu wa ajabu katika maisha yangu.

Bibi yangu alizaliwa katika Kitongoji cha Butimba, Kijiji cha Kome, Kata ya Bwasi, Tarafa ya Nyanja (Majita), Wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara, katika familia ya watoto kumi, mwaka 1930. Alisoma katika Shule ya Msingi ya Kome ambako alipata elimu ya awali na msingi na pia elimu ya kiroho kwani shule yao ilikuwa ya madhehebu ya Kisabato. Aliolewa na Bwana Maregesi Musyangi Sabi mwaka 1946, na kufanikiwa kupata watoto watatu; wa kiume wakiwa wawili na wa kike mmoja. Matatizo hasa ya bibi yalianza mwaka 2005, alipougua kiharusi akiwa nyumbani kwake huko Musoma. Hata hivyo alitibiwa hapo Musoma na Dar es Salaam akapona na kuwa mwenye afya ya kawaida. Lakini tarehe 19/10/2014 alipatwa tena na kiharusi na kulazwa tena katika Hospitali ya Mkoa ya Musoma, ila akajisikia nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani – lakini kwa maagizo ya daktari ya kuendelea na dawa akiwa nje ya hospitali. Tarehe 29/10/2014 alirudi tena Hospitali ya Mkoa ya Musoma kwa tiba zaidi, lakini tarehe 4/11/2014 saa 7:55 usiku akafariki dunia; akiwa amezungukwa na familia yake.

Dunia ina watu wachache sana wenye matumaini na misimamo ya kutegemea mazuri, na wachache zaidi ambao wako tayari kugawa matumaini na misimamo hiyo kwa watu wengine. Nitajisikia furaha siku zote kwamba miongoni mwa watu hao wachache, hata bibi yangu alikuwemo. Msalaba uliwekwa wakfu na Mwenyezi Mungu baada ya mwili wa Yesu Kristo kuning’inizwa juu yake. Kwa kuwa bibi yangu ametanguliwa na msalaba, msalaba utamwongoza mahali pa kwenda.
Enock Maregesi
01-55-hours19-10-20141930